The United Republic of Tanzania | Ministry of Information, Communication and Information Technology | ICT Commission
 INFORMATION AND COMMUNICATION TECHNOLOGY COMMISSION


Media Centre

Speech


Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa(MP) - Prime Minister of United Republic of Tanzania

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee!

Tanzania Oyee, haya tukae!

Mheshimiwa Jerry Slaa, Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Marry Prisca Mavundi, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Godfrey Mollel, Naibu Waziri wa Afya, Ndugu Mohammed Hamis Abdula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, Ndugu Nicholas Mkapa, Naibu Katibu Mkuu wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari.

Natambua uwepo wa makatibu wakuu kutoka wizara mbalimbali na manaibu katibu wakuu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama waliopo hapa. Dr. Nkundwe Moses Mwasaga, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Menejimenti, Wawakilishi wa wizara na taasisi mbalimbali za serikali, Mheshimiwa Suleiman Kakoso, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Waheshimiwa Wabunge, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia miundombinu, Waheshimiwa Mabalozi kutoka nchi mbalimbali, Bwana Tobias Makoba, Mkurugenzi Mkuu wa Habari na Msemaji wa Serikali, uongozi na uwakilishi wa makampuni mbalimbali ya TEHAMA, wawekezaji wa miundombinu na huduma za TEHAMA waliopo hapa ndani, wataalamu mbalimbali wa TEHAMA ambao pia mko nasi, wabunifu wa huduma za kidijitali, tumewaona kwenye mabanda, viongozi wa madhehebu ya dini tunawashukuru kwa dua zenu, wanahabari, mabibi na mabwana… Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee!

Ndugu washiriki, na mimi niungane na viongozi wa dini kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kukutana hapa jijini Dar es Salaam, Tanzania, tukiwa tumetoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya kuhudhuria Kongamano la Nane la Mwaka 2024 la TEHAMA hapa jijini Dar es Salaam. Lakini pia, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Jerry Slaa, Waziri wa TEHAMA, kwa kusimamia vyema dhamana ya habari, mawasiliano, na teknolojia ya habari, pamoja na maandalizi ya kongamano hili muhimu.

Nafahamu kwamba mafanikio katika sekta unayoisimamia, Mheshimiwa Waziri, yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati yako, timu yako ya wizara, pamoja na viongozi mbalimbali kutoka sekta binafsi. Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana sekta binafsi kwa ushiriki wenu na kwa kuiunga mkono serikali yetu kwenye maandalizi ya kongamano hili. Pia, niendelee kuwapongeza washiriki wote kwa kutenga muda wenu na kuja kushiriki katika kongamano hili la kipekee.

Ninatambua kwamba hapa ndani tunao wageni kutoka nchi mbalimbali, na nawashukuru kwa kuja na ninawakaribisha wote. Pia nawasihi muendelee kushiriki nasi katika shughuli mbalimbali zilizopangwa kwa baadaye. Kwa kipekee kabisa, natoa shukrani za dhati kwa AUDA-NEPAD, ambao ndio walipendekeza Tanzania iwe mwenyeji wa kwanza wa mashindano ya vijana wa Afrika na kuonyesha ubunifu wao katika matumizi ya akili mnemba na roboti. Ninakiri kwamba hii ni fursa muhimu sana, na mimi nimepata nafasi ya kupita kwenye mabanda ya maonyesho na kuona jinsi vijana wa Tanzania na Bara la Afrika walivyoweza kubuni njia mbalimbali, hasa kwenye matumizi ya akili mnemba na roboti. Hongereni sana!

Ndugu washiriki, ni matarajio yangu kwamba wataalamu wote waliopo kwenye kongamano hili la nane mmejadili mambo mengi katika kipindi mlipokaa hapa, na yote mliojadili yamejikita katika namna teknolojia itakavyoweza kutumika kuleta mapinduzi ya viwanda ya nne, tano, na sita, na hatimaye kuondoa mitizamo kinzani iliyopo katika jamii yetu.

Ndugu washiriki, kama mnavyofahamu, Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan ndiye aliyekuwa amealikwa kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hili. Kutokana na majukumu yake mengi ya kitaifa, ameniagiza kuja kumwakilisha. Pamoja na kuniagiza kumwakilisha, ametuma salamu nyingi sana kwenu, akiwatakia kila la kheri katika kongamano hili, ambalo anaamini limekuwa na mafanikio. Mmefanya mapitio ya maeneo yote muhimu, mafanikio yenu, changamoto zenu, na pia mmekuja na hatua au suluhisho za changamoto hizo, hasa katika matumizi ya TEHAMA. Salamu hizi zinajumuisha pia salamu kutoka kwa Mheshimiwa Dr. Phillip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye naye ana imani kwamba kongamano hili limetoa suluhisho zinazohitajika kufuatia changamoto mlizokabiliana nazo katika kipindi kilichopita, kuhusu masuala ya TEHAMA.

Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, nitumie nafasi hii kuwakaribisha wageni wetu wote. Karibuni sana Tanzania, nchi yetu iko salama, Watanzania wana upendo, na ni wakarimu. Watanzania wanajivunia kuwa na ninyi hapa, kwani mnapata nafasi ya kubadilishana uzoefu, hasa katika masuala ya TEHAMA. Karibuni sana wote hapa nchini!

Ndugu washiriki, moja ya mambo yanayovutia katika kongamano hili ni kauli mbiu yake: Kutumia uwezo wa akili mnemba na roboti kwa ajili ya mapinduzi ya kiuchumi na kijamii. Kauli mbiu hii ni halisi kwa sababu inawiana na azma ya serikali ya awamu ya sita, ya kuleta tija kwa wananchi kupitia mabadiliko ya teknolojia.

Kauli mbiu hii imekuja wakati muafaka ambapo dunia inafanya jitihada kubwa za kukuza teknolojia na kuongeza matumizi yake ili kuinua uchumi na ustawi wa jamii yetu. Kama mnavyofahamu, dunia inazidi kupiga hatua kwenye matumizi ya TEHAMA, ambayo yanachochea mapinduzi ya viwanda ya 4, 5, na 6. Sina shaka kwamba sote tunaendelea kushuhudia mabadiliko haya ya teknolojia katika maeneo tulipo, na tofauti kubwa kutoka tulikotoka. Pia, kuibuka kwa teknolojia kama akili mnemba na roboti kumeweka ajenda muhimu katika kila sekta.

Kutokana na ukweli huo, ni lazima taifa kujipanga vizuri ili kuendana na mabadiliko haya ya teknolojia bila kuathiri misingi tuliyonayo. Ndugu washiriki, nitumie nafasi hii kueleza jitihada za serikali yetu ya awamu ya sita katika kuimarisha TEHAMA. Serikali yetu, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu, inatambua umuhimu wa TEHAMA katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii. Kwa hivyo, serikali inafanya jitihada makusudi kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na matumizi ya TEHAMA.

Moja ya jitihada hizo ni kujenga mifumo muhimu ya uendeshaji pamoja na mazingira wezeshi, ikianza na kisera na kisheria. Sheria hizi zimeunda kanuni ndani ya kila taasisi ili kuendeleza mifumo muhimu. Kama mnavyojua, serikali imekuwa ikiandaa makongamano ya kitaaluma ili kuhakikisha maarifa na ujuzi wa wana TEHAMA vinaongezeka. Natoa pongezi kwa Tume ya TEHAMA na Mkurugenzi Mkuu kwa kusimamia vyema masuala ya TEHAMA na maendeleo ya sekta hii nchini.

Jitihada zenu zimezaa matunda, na nilipita kwenye mabanda ya maonyesho na kuona mabadiliko makubwa sana. Mabanda mengi yalionyesha ubunifu wao, na kila ubunifu ulikuwa unaonyesha maendeleo kutoka miaka ya nyuma na hatua ambazo tumefikia sasa. Hongereni sana Mkurugenzi wa TEHAMA na taasisi yako kwa mafanikio haya!

Ndugu washiriki, sambamba na jitihada hizi, serikali tayari imeanzisha Bodi ya Ithibati na imeandaa mpango mkakati wa miaka 5, unaoanza mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2029/2030. Huu ni mkakati wa kuendeleza masuala ya anga za juu. Serikali inaendelea kutekeleza programu hii ili kufikia malengo ambayo tunatamani kuyaona.

Nimefarijika sana kusikia kwamba Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) imefanikiwa kupata mradi mkubwa wa utafiti wa kuwezesha kurusha satellite, kupitia mradi unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa kupitia shirika linalosimamia masuala ya anga za juu, United Nations Office for Outer Space Affairs (UNOOSA), kwa kushirikiana na Taasisi ya Anga za Juu ya Japan (JACSA). Hii ni hatua kubwa sana kwa taifa letu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuinua sekta ya teknolojia nchini.

Serikali pia inaendelea na utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi, ambao umekuwa wa manufaa makubwa kwa taifa. Kutokana na jitihada hizi, tumeona ongezeko la ukuaji wa huduma za TEHAMA, ikiwemo utumiaji wa huduma za simu kwa kasi zaidi. Hii inaonyesha jinsi serikali inavyoweka msisitizo mkubwa katika kukuza sekta ya teknolojia nchini.

Ndugu washiriki, kama mtakumbuka, Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizindua mkakati wa kiuchumi wa kidigitali. Moja ya nguzo muhimu katika mkakati huo ni utambuzi wa raia, ambao utawezesha utoaji wa huduma kwa njia za kidigitali. Ili kuhakikisha mkakati huu unatekelezwa kwa mafanikio, imepangwa kuwa kila raia awe na namba ya pekee ya utambulisho itakayomuwezesha kupata huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii, kutoka serikalini na hata sekta binafsi.

Serikali imeweka wazi kuwa Namba ya NIDA ndiyo itakuwa Namba Jamii, ambayo itatumika kwa utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali hapa nchini. Kwa msingi huu, nawahimiza Watanzania wenzangu kuhakikisha mnapata Namba ya NIDA ili muweze kufaidika na huduma hizi.

Lengo la serikali ni kuhakikisha kila mmoja anatambulika, sambamba na kutambua sekta rasmi ili kufikia matumizi ya kidigitali katika nyanja mbalimbali hapa nchini. Hatua hii itasaidia sana katika kuchangia pato la taifa letu. Pia, hatua hii itachochea kupunguza matumizi ya fedha taslimu, kwani watu wataweza kulipa kwa kutumia namba hiyo hiyo. Hii itapunguza hatari za unyang'anyi wa fedha taslimu na changamoto zingine zinazotokana na kushika fedha.

Tutaanzisha utaratibu wa kutumia QR Codes, ambao utachochea ukuaji wa uchumi wa kidigitali. Kwa hivyo, nawasihi Watanzania kuhakikisha wanapata vifaa vya kidigitali kama vile simu na kadi za kielektroniki, ili kufikia hatua ambayo tunahitaji kama taifa.

Ndugu washiriki, lengo la namba hii ya jamii ni kuifanya mifumo ya TEHAMA kusomana na kubadilishana taarifa kwa urahisi. Mifumo ikisomana, inarahisisha utoaji wa huduma za kijamii, kiuchumi, na hata kiusalama. Hii itakuwa rahisi kwa watumiaji wote, kwani ukiwa na namba hii pamoja na kadi yako, itakuwa rahisi kufanya mawasiliano kwenye sekta zote, iwe ni sekta za kifedha au nyinginezo, hivyo kurahisisha mawasiliano na huduma kwa wananchi.

Kutokana na umuhimu huo, taasisi za umma na binafsi zinapaswa kuhakikisha kwamba mifumo yao yote ya ndani inasomana, na lazima zibadilishane taarifa na NIDA ili kufikia lengo lililokusudiwa. Hii inajumuisha pia sekta binafsi. Wewe kama mtumishi wa umma, unaweza kuwasiliana na kampuni inayouza bidhaa au huduma mbalimbali. Mfano mzuri ni taasisi kama mabenki na maeneo yote yanayohitaji kupata na kutoa taarifa.

Serikali kwa upande wetu, tunaendelea kuboresha mfumo wa kubadilishana taarifa, ujulikanao kama Jamii Exchange, ambao upo chini ya Wizara ya ICT. Ni muhimu wote kuhakikisha utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais la kuunganisha mifumo yote unakamilishwa kwa wakati uliopangwa.

Ndugu washiriki, mabadiliko ya kidigitali hayakwepeki kwa sasa. Safari hii ya mabadiliko ya kidigitali haitamuacha mtu yeyote nyuma, hususan katika mfumo wa kifedha jumuishi, ambao ni muhimu sana.

Kama mnakumbuka, serikali ilizindua mfumo wa N-Card mwaka 2020, na hadi sasa umeweza kuunganisha wananchi zaidi ya milioni 4. Mfumo huu umesaidia sana kuokoa fedha ambazo zingepotea kwenye vituo vya usafiri kama vile Magogoni kwenye kivuko, na pia kwenye viwanja vya michezo. Wanunuzi wa tiketi za michezo hutumia N-Card, ambapo tiketi hutangazwa wiki kadhaa kabla ya mechi na zinapouzwa zote, uwanja unajaa kabisa kabla ya siku ya tukio.

Mfumo huu umeongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo mbalimbali, mfano, Magufuli Bus Terminal na viwanja vya michezo, na hii ni hatua kubwa ambayo tunapaswa kujipongeza kama Watanzania kwa sababu tumeenda mbele zaidi.

Ninatoa wito kwa Wizara kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo serikali imewekeza na yanahitaji kutumia mfumo wa N-Card, ambao sasa mmeuita Jamii Card, yanafuata utaratibu. Mfumo huu ni muhimu sana katika kuokoa upotevu wa fedha za serikali na kuwasaidia wananchi kutotembea na fedha taslimu, badala yake kutumia fedha kidigitali.

Endeleeni kufuatilia matumizi ya mifumo hii na kuhakikisha inaimarishwa, huku mkipanua wigo wa mifumo ya taasisi za ndani na nje ili ziweze kusomana.

Ndugu washiriki, masuala ya Tehama ni mtambuka, na huu ni msukumo kwa kila nchi, jumuiya za kikanda, na kimataifa kuendelea kuandaa mipango mbalimbali kuhusu teknolojia zinazochipukia. Umoja wa Afrika tayari umeweka mikakati inayochochea matumizi ya teknolojia hizi pamoja na kuendeleza ujuzi na utaalamu. Katika eneo hili, tafiti na uwekezaji vinahitajika kwa kiwango kikubwa.

Taifa letu, kama sehemu ya jumuiya hizi za kikanda na kimataifa, lina wajibu wa kubuni mikakati mbalimbali na kuhakikisha tunakwenda sambamba na maendeleo haya ya teknolojia ili tusiachwe nyuma. Leo tunapoenda katika nchi nyingine, tunaona wenzetu hawatumii fedha taslimu madukani, wanatumia kadi. Wakati mwingine tunaona kama changamoto, lakini hatuna sababu ya kuendelea kuachwa nyuma. Tunatakiwa kwenda kwa kasi sawa na wao ili tuweze kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa kidigitali.

Kwa hiyo, nawaagiza wataalamu wetu, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, e-GA, na Katibu Mkuu wa Wizara kuhakikisha kwamba hili linakamilika haraka. Lengo ni kwamba kila Mtanzania awe na kadi ambayo ataweza kuitumia kwenye matumizi yake ya kila siku, na fedha zitaendelea kubaki benki kwa usalama.

Ripoti za sasa zinaonyesha kuwa katika karne ya 21, matumizi ya akili mnemba na robots yanazidi kuongezeka kwa kasi. Ili kufikia malengo ya ajenda ya mwaka 2030 na mkakati wa uchumi wa kidigitali wa mwaka 2034, tunahitaji kuongeza juhudi na ubunifu zaidi katika matumizi ya teknolojia hizi ili kutoa huduma bora na zenye ufanisi zaidi. Hii ni fursa muhimu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa kidigitali si tu hapa nchini, bali pia kwa nchi nyingine za Afrika ambazo tayari zimeshaingia kwenye uchumi huu.

Nimefurahi sana leo kuona vijana wa Kiafrika wakipewa zawadi kwa ushindi wao kutokana na tafiti na mifumo ya kidigitali waliyoibuni, ambayo tayari inafanya kazi. Tunawatia moyo vijana wengine kuendelea kuwa wabunifu, huku serikali ikiendelea kukamilisha jengo la wabunifu wa kidigitali, ambapo kila mmoja atakuwa na fursa ya kuingia na kufanyia kazi mawazo yake.

Nimefurahi pia kuona Wizara ya ICT imetengeneza mfumo ambapo mtu na ubunifu wake anaweza kuuweka kwenye mfumo, na vijana wengine wakaona ubunifu huo, wakatoa mchango wao. Kila mmoja anaweza kuchangia mawazo ya namna ya kuboresha zaidi na kupata kitu bora zaidi. Haya ndiyo maendeleo tunayoyahitaji!

Hii mifumo ya N-Card na mingine ambayo tumeanza kutumia sasa imetengenezwa na Watanzania wenyewe. Nataka niwaeleze jambo, mwaka 2016/2017 nilienda Kenya, na mwaka 2019, nilienda Rwanda. Kenya wameweza kutengeneza iPads, yaani vishkwambi, na mtaalamu aliyetengeneza hicho kishkwambi ni Mtanzania. Hata yule aliyeenda Rwanda, ni Mtanzania. Wamefanikiwa kutengeneza vishkwambi, lakini sisi ambao tumewazalisha wataalamu hawa, bado hatujatengeneza vyetu.

Sasa ni wakati wa kwenda kwa kasi sana. Lazima twende spidi na sisi wenyewe tutengeneze vyetu, kupitia wataalamu wetu kwa sababu tumeshadhihirisha uwezo wetu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kama tumetoa wataalamu walioenda kutengeneza Rwanda na Kenya, kwanini sisi wenyewe tusitengeneze?

Wizara, tafadhali tengenezeni mpango mkakati wa kuwapata vijana wabunifu ambao wanaweza kubuni teknolojia zenye tija. Lakini pia simamieni tafiti zinazofanyika na zinatoa matokeo, ili wataalamu wetu wapate fursa za kutengeneza bidhaa ambazo zitafika kwa jamii na kuanza kutumika.

Ndugu washiriki, ni wazi kuwa jitihada nyingi zinafanywa na nchi za Kiafrika kupanua wigo wa matumizi ya teknolojia, na zinaleta mfano mzuri kwa nchi nyingine ambazo bado hazijaanza kuiga. Mfano mzuri ni utoaji wa vitambulisho vya kidigitali, ujenzi wa miji janja (smart cities), na uboreshaji wa huduma za afya, usalama, kilimo, na mengine mengi, kama ambavyo leo tunashuhudia ushindi wa wabunifu waliogusa maeneo haya. Huu ni ushahidi kwamba teknolojia zinazoibuka zinatoa fursa kwa serikali na wadau wengine kupanga mikakati mipya kwa ajili ya wananchi wetu.

Tafiti zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2030, shughuli nyingi za kijadi zitaboreshwa na kufanywa kidigitali. Matumizi ya teknolojia hizi yanaweza kuleta changamoto za kiutamaduni, kimaadili, na masuala ya faragha, lakini hatuwezi kuachwa nyuma kwa hofu ya changamoto hizi. Muhimu ni kuhakikisha sera, sheria, na kanuni zinaboreshwa ili kulinda watumiaji wa kidigitali, kuzuia matumizi mabaya, na kuheshimu mila na desturi zetu. Hili ni jambo muhimu sana.

Kutokana na hayo, serikali na wadau wote lazima tuwe na mikakati thabiti, kama mnavyofanya leo kwenye kongamano hili. Ni muhimu kuzingatia masuala ya matumizi mabaya ya kidigitali yanayofanywa na wachache, ambayo yanaweza kuharibu mwelekeo wa teknolojia hii.

Serikali kwa kutambua hili, imeendelea kuweka mifumo ya kisera, sheria, na taasisi kama ifuatavyo:

Kwanza, imefanya mapitio ya Sera ya Tehama ya mwaka 2016 kwa kuongeza masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na teknolojia zinazoibuka na startups kwenye masuala ya Tehama. Maandalizi ya kutunga sheria maalum za Tehama yanaendelea, na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mheshimiwa Kakoso, ameeleza kuwa tayari zipo sheria ambazo zimeshasomwa kwa mara ya kwanza ili tupate sheria kamili kwenye eneo la Tehama. Kamati hiyo na wabunge wataendelea kushirikiana kwa ajili ya maboresho ya sheria hizo.

Wadau wamepata nafasi ya kuchangia, na wataendelea kuchangia huku maboresho yakiendelea kufanyika. Kamati chini ya mwenyekiti na waheshimiwa wabunge waliopo hapa wataendelea kuhakikisha kwamba hili ni jukumu letu ndani ya Bunge. Hili ni jambo ambalo linahitaji ushirikiano na umakini mkubwa.

Pili, tumeanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Hatua hii ni muhimu sana, hasa katika nyakati hizi ambapo teknolojia zinavyoendelea kukua, masuala ya faragha na usalama wa taarifa yanazidi kuwa ya muhimu. Tume imejiimarisha kwenye eneo hili ili kuhakikisha taarifa za watu binafsi zinapata ulinzi wa kutosha. Tume hii itaendelea kufuatilia kwa karibu ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi mabaya ya taarifa za kibinafsi.

Tatu, kwenye maboresho ya kisera na sheria, tumeandaa mkakati wa uchumi wa kidigitali, unaojulikana kama Tanzania Digital Economic Strategy Framework kwa miaka 10, kuanzia mwaka 2024 hadi 2034. Mkakati huu umebainisha malengo mbalimbali ambayo kama nchi tunatarajia kuyatekeleza ili kufikia uchumi wa kidigitali. Huu ni msingi wa maendeleo ya kidigitali nchini, na unatoa mwongozo kwa serikali na wadau wake kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ambayo ina uwezo wa kubeba teknolojia mpya zinazoibuka. Teknolojia hizi, ambazo tayari zimefanyiwa utafiti, zinatakiwa kuendana na mahitaji ya sasa ya kijamii na kiuchumi.

Tunataka tuimarishe zaidi tafiti hizi ili zichangie kwenye maendeleo ya teknolojia nchini, pamoja na kuchochea uwepo wa ubunifu mbalimbali wa kidigitali unaolingana na mahitaji halisi ya wakati huu. Hatua hizi pia zitaimarisha usalama wa mifumo na data zetu, jambo ambalo ni msingi muhimu kwa maendeleo ya teknolojia na uchumi wa kidigitali kwa ujumla.

Nne, kuwekeza rasilimali nyingi katika kukuza tafiti ni eneo ambalo tumeweka msisitizo mkubwa kwa sababu linatoa fursa kwa vijana wa Kitanzania kubuni kazi mbalimbali, bila kujali umri wao. Wanafunzi kutoka shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu, na vyuo vya kati wote wanapaswa kushiriki katika ubunifu huu.

Ninataka tuendelee kuwahamasisha vijana hawa kufanya ubunifu, hasa katika bidhaa mpya za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama). Ni muhimu kuanzisha vituo vya Umahiri vya Tehama, ICT Centres. Ili kufanikisha jambo hili, serikali tayari imeshadhamiria kuanzisha chuo maalum cha ubunifu wa Tehama ndani ya jiji la Dodoma na mkoani Kigoma. Hatua hii inalenga kutanua wigo wa matumizi ya Tehama, na itachochea sana shughuli za kiuchumi na kijamii, hivyo kuchangia maendeleo ya taifa letu.

Kama nilivyotangulia kusema, kazi kubwa tayari imeshafanywa, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa utambuzi wa kidigitali ambao umepewa jina la Jamii Number, utakaotumika katika mifumo ya kutolea huduma. Serikali itaendelea kuijengea uwezo Tume ya Tehama ili iweze kuendelea kuratibu na kuhamasisha shughuli mbalimbali za ubunifu za kidigitali kote nchini. Hii ni kazi muhimu ya Tume yetu ya Tehama.

Kama ambavyo mmeona, Tume imeanza kazi yake vyema, na ni matarajio yetu kwamba serikali itaongeza msukumo katika kuhakikisha tunafikia mapinduzi ya kidigitali. Mkurugenzi Mkuu alivyokuja hapa, alieleza kwamba kongamano hili lilikuwa na malengo ya kuhamasisha na kutoa mwanga juu ya sekta ya kidigitali. Natoa wito kwa kila mmoja wenu kuhakikisha anajitolea na kujiunga na mapinduzi haya ya kidigitali, kwa ajili ya maendeleo yetu sote.

Kabla sijahitimisha hotuba yangu, nitumie nafasi hii kuweka msisitizo katika maeneo mengine kadhaa. Eneo la kwanza, Wizara, hakikisheni matumizi ya Tehama katika kutoa huduma yanaimarika. Biashara na uzalishaji lazima uongezeke, uwazi wake, ufanisi, na uboreshaji wa maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii ni jukumu mnatakiwa kulisimamia.

Pili, Wizara pamoja na wadau wote tekelezeni maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais kuhusu kuunganisha mifumo yote ya Tehama. Kuna haja ya kufuatilia sasa, kila taasisi je, imeunganisha mifumo na serikali? Tuanze na taasisi ambazo tunafanya nazo kazi wakati wote, hiyo ni mahali pa kuanzia. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumejiunganisha vizuri.

Tatu, Wizara ikishirikiana na Wizara ya Nishati, itekelezeni kwa wakati ujenzi wa Chuo cha Tehama mkoani Kigoma ili kianze kazi yake. Wizara ya Nishati nayo ina mpango wa kuimarisha chuo hicho kwa pamoja nanyi.

Wizara vilevile inapaswa kusimamia na kuhakikisha ujenzi wa vituo vya ubunifu (Innovation Hubs) katika mikoa iliyokubalika kuanzishwa. Mtenge bajeti inayohitajika, na kama mnashirikisha mamlaka ya serikali za mitaa, mfanye hivyo ili kujenga hizo hubs kwenye mikoa yetu. Hili litasaidia kuharakisha kuwa na majengo mara moja!

Kwa Tume ya Tehama, kamilisheni mchakato wa kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya Tehama, yani ICT Refurbishment and Assembly Centre. Hakikisheni hilo, kwa sababu programu mnayo!

Tume, muendelee kuboresha mfumo wa kuwatambua na kuwasajili wataalamu wa Tehama nchini. Ni lazima tuwe na mfumo wa kuwatambua wataalamu hawa. Wengi waliokuwepo hapa hawatambuliki kama wataalamu wa Tehama, hivyo lazima mbuni mfumo huo. Kama mlieshaanza, vizuri. Na kama hamjaanza, anza sasa. Muanze tu na hawa walio kwenye kongamano, msajili hawa kwanza pamoja na wale walioshinda.

Wanapata nafasi ya kutafuta viongozi wao kwa kuanzia. Lakini kama mmeshafanya, muendelee. Ni muhimu muwaandikishe tuwatambue wako wapi na wanafanya nini.

Muweke mkakati wa kutembelea kwenye mashule huko, kuhamasisha vijana walioko shuleni: vyuo vikuu, vyuo vya kati, kwenye ngazi za sekondari ya juu na ile ya chini, pia shule za msingi. Hii itasaidia sana kuhakikisha kuwa tunatambua na kuwaibua wengine. Aidha, tembeleeni maonyesho yanayoandaliwa na Wizara ya Elimu, yale ya ubunifu ambapo vijana wengi hutengeneza kazi zao.

Kwa wananchi ambao hawajapata namba za NIDA, muende mkajiandikishe sasa. Namba hii ni muhimu sana, hususani katika wakati huu tunapoanza kutumia mifumo ya digitali ambayo inasomana na NIDA. Ni muhimu kwenda kujiandikisha ila nawe pia usiachwe nyuma.

Kwa hiyo, ndugu washiriki, yale niliyoyaeleza hapa ni muhimu yasimamiwe na tunataka tuone matokeo. Wakati ule, tukiwa tunataka mrejesho, tupate mrejesho.

Natambua kuwa mmenisikia, mmejifunza mengi, na mmejadili kupitia kongamano lenu. Sisi kwa upande wa serikali, kupitia Wizara, tunasubiri mapendekezo yenu ambayo mmeandaa.

Kupitia hotuba yangu, ntakuwa mchoyo wa fadhila kama sitowashukuru kipekee kabisa wadhamini wote wa kongamano hili, kama ambavyo walitamkwa. Katibu Mkuu, na mimi nawapongeza, kwa sababu kongamano limefanikiwa kuwa na idadi kubwa ya washiriki. Ni mafanikio.

Na ninaamini, nyie ni wataalamu; kukusanyika kwenu hapa kumeweza kusimamia utaalamu wenu na mmejadili mambo mengi.

Kwa hiyo, baada ya kusema hayo, nataka kutangaza rasmi kwamba kongamano la nane la mwaka wa Tehama nchini Tanzania kwa mwaka 2024, limefungwa rasmi!

Asante sana!

 

036A0649