The United Republic of Tanzania | Ministry of Information, Communication and Information Technology | ICT Commission
 INFORMATION AND COMMUNICATION TECHNOLOGY COMMISSION


Media Centre

Speech


Honourable Jerry William Silaa(M.P) - Minister of Information Communication and Information Technology

Mheshimiwa Waziri Mkuu, Viongozi wa Meza Kuu, Washiriki wa Kongamano, Mabibi na Mabwana. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee!

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kushiriki kilele cha Kongamano la Nane la Mwaka wa Tehama. Pia ningependa kutoa shukrani za dhati kwako, Waziri Mkuu, kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi kwenye kilele cha kongamano hili. Tunakushukuru sana!

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tulikuwa tumeandaa hotuba fupi ya kukukaribisha, lakini niseme kwa dhati, umekuja mapema na mengi tuliyopanga kuyasema umeyaona tayari kwenye mabanda. Wazungumzaji waliotangulia wamesema mengi, na vile vile tuliwasilisha presentation kwa njia ya video iliyozungumzia mafanikio makubwa ya kisekta ndani ya Wizara ninayoisimamia. Ukianzia na upatikanaji wa mtandao wa simu nchini, tumefikia asilimia 89 kwa mtandao wa 3G na asilimia 84 kwa mtandao wa 4G. Mtandao wa mkongo wa taifa umeenea hadi kilomita 13,820, na mtandao wa makampuni ya simu kupitia mfumo wa Corsoteum umejengwa kwa kilomita 1,592.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kituo chetu cha mawasiliano na uhifadhi wa data, NIDC, tayari kimehamishiwa TTCL. Pia napenda kukuarifu kuwa Wizara imeanza maandalizi ya urushaji wa satellite, na mkakati wa miaka mitano kwa programu za anga za juu umeanza kuandaliwa. Haya maandalizi yanahusisha utungwaji wa sera, sheria, na mikataba ya kimataifa kuhusiana na masuala ya anga za juu.

Kwa upande wa miradi, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) imepata mradi wa utafiti wa kuwezesha urushaji wa satellite kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa kupitia taasisi ya United Nations Office for Outer Space Affairs (UNOSA) pamoja na Taasisi ya Anga za Juu ya Japan (JACSA).

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, umeona pia kwenye banda la Wizara mfumo wa Anwani za Makazi (NAPA) na faida zake kwa taifa letu. Vilevile, umejionea jinsi Wizara inavyotekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha mifumo inasomana, kama vile Jamii Number, Jamii Malipo, na Jamii Exchange.

Kongamano hili la nane limefanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Kutumia Uwezo wa Akili Bandia na Robotics kwa Ajili ya Mapinduzi ya Kiuchumi na Kijamii.” Kama ulivyopokea taarifa, kongamano limefanyika kuanzia Jumapili, na leo tumekualika kulifunga. Kaulimbiu hii inaweka msingi wa matumizi ya teknolojia zinazoibukia, kama vile akili bandia, robotics, na uchambuzi wa Big Data, katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, leo hii utatoa tuzo kwa washindi wa mashindano ya vijana wa Afrika kuhusu Robotics na Akili Bandia (Artificial Intelligence and Robotics Competition). Pia, utatoa tuzo kwa vijana wa Kitanzania waliopata mafanikio kwenye mashindano ya kimataifa kuhusu teknolojia hizi. Hii ni fursa kubwa kwa taifa letu, kwani mashindano haya yanafanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika, na Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa kilele cha mashindano haya, yaliyoratibiwa na Taasisi ya Maendeleo ya Afrika (AUDA–NEPAD).

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Serikali imeanza ujenzi wa Chuo cha Teknolojia ya Kidigitali (Digital Technology Institute) kule Nala, Dodoma, ambacho kitakuwa kituo cha mafunzo ya vitendo kwenye teknolojia zinazoibukia.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kazi yangu kubwa ni kukuomba masuala yafuatayo:

       Tunakuomba upokee zawadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoka AUDA–NEPAD.

       Tunakuomba upokee zawadi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, ambayo ni mfano wa chuo kitakachojengwa Nala, Dodoma. Tunakuomba utuombee kwa Mheshimiwa Rais ili chuo hiki kiitwe Dr. Samia Suluhu Hassan Digital Technology Institute.

       Tunakuomba upokee zawadi yako kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, ambayo ni mfano wa satellite, ikiwa ni ishara ya mwanzo wa safari ya utekelezaji wa programu ya miaka mitano ya masuala ya anga za juu, ijulikanayo kama "From Mount Kilimanjaro, the Peak of Africa, to Space."

       Tunakuomba utoe tuzo, vyeti, na zawadi kwa washindi.

       Mwisho, tunakuomba ulihutubie hadhara hii iliyokusanyika mbele yako.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa heshima na taadhima, sasa nakukaribisha kuanza na shughuli hizo niliyotangulia kuyataja, na baada ya hapo uzungumze na hadhara iliyoko hapa. Mheshimiwa Waziri Mkuu, karibu sana!

Mshereheshaji kisha alimkaribisha Waziri Mkuu kwa ajili ya kuanza shughuli za utoaji wa zawadi, akianza na zawadi ya kwanza mpaka zawadi kwa Waziri Mkuu.

Baada ya hapo, Mshereheshaji (M.C) alimkaribisha Dada Yvonne kutoa maelezo mafupi kabla ya kuanza kwa shughuli za utoaji zawadi.

036A0514